ASKARI WA WANYAMA PORI AUAWA KIKATILI _--MOROGORO
Askari
wa wanyamapori wa hifadhi ya mbuga ya Jukumu iliyoko katika Wilaya ya
Morogoro, ameuawa kikatili na wengine kujeruhia baada ya kuvamiwa na
kundi la wafugaji jamii ya Kisukuma.
Baadhi ya askari
waliojeruhiwa, Yahaya Ramadhani na Khalphan Shabani, walisema tukio hilo
lilitokea juzi wakati askari hao wakiwa katika doria nyakati za usiku
katika mbuga hiyo.
Kwa upande wake, Shabani alisema kuwa wakati
wakiwa katika doria hiyo, ghafla walivamiwa na kundi la wafugaji wa
jamii ya Kisukuma na kuanza kushambuliwa kwa silaha za aina mbalimbali
ikiwamo mikuki na marungu na kusababisha kifo cha askari mwenzao.
Alimtaja askari aliyefariki dunia baada ya kuchomwa mkuki kuwa ni Ramadhani Magengere, ambapo askari watatu walijeruhiwa.
Kwa mujibu wa Shabani, hilo ni tukio la tatu kutokea katika mbuga hiyo.
Hata
hivyo, askari huyo wa wanyamapori, alilishutumu Jeshi la Polisi mkoani
Morogoro kwa kushindwa kutoa ushirikiano kuhusiana na mauaji hayo licha
ya kutolewa taarifa.
Ofisa Maliasili Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Chuwa
alisema hilo ni tukio la sita kwa askari wa wanyamapori kujeruhiwa hadi
kusababisha kifo huku Jeshi la Polisi kutokutoa uzito wa matukio hayo
licha ya kupewa taarifa.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro,
Faustine Shilogile, pia alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza
kwamba uchunguzi unaendelea wa kuwatafuta wahusika.
Hata hivyo, Kamanda Shilogile aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kupatikana kwa wahusika hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni