Moshi.
Mwandishi wetu.
Serikali imefikia maazimio saba yatakayowawezesha waongoza utalii na wapagazi kupata ujira wao stahiki na kwa wakati.
Katibu mteule wa Chama cha Waongoza Utalii (TGA), James Mong’ateko alisema hayo mjini Moshi jana.
Alisema miongoni mwa maazimio hayo ni wapagazi kulipwa asilimia 50 ya ujira wao kabla ya kuanza kufanya kazi.
“Hii
ni sahihi kabisa wapagazi kabla ya kuanza safari zao ambazo huchukua
kati ya siku saba hadi nane wataweza kuacha nyumbani fedha za matumizi,”
alisema.
Alitaja maazimio mengine kuwa ni Wizara ya
Maliasili na Utalii kupitia Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kuzuia kampuni
ambazo hazijasajiliwa kutoa huduma kwa watalii.
Alisema
utekelezaji wa maazimio hayo utasaidia waongoza watalii na wapagazi
kulipwa mishahara yao halali kwa mujibu wa Tangazo la Serikali, GN 228.
“Kulikuwa
na kisingizio ya kuwa gharama kubwa za leseni wanazotozwa kampuni ya
utalii ndiyo chanzo cha wao kuwalipa ujira ulio nje ya agizo la
Serikali, lakini kwa azimio hili gharama hizo hazitakuwa sababu tena ya
kunyimwa haki zetu za msingi,” alisema Mong’ateko.
Mwenyekiti
wa TGA, Sadock Johnson aliiomba Serikali kupitia mamlaka zake husika
kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa kama ilivyoafikiwa na pande
zote.
Wakili wa TGA, Elikunda Kipoko alisema wataunda kikosi kazi kitakachofuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio hayo saba.
“Haina
haja ya kumtafuta mchawi katika kukabiliana na changamoto
zinazowakabili waongoza utalii na wapagazi tena, baada ya maazimio haya
kupatikana kikubwa ni kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika haraka kwa
manufaa ya wahusika,” alisema Kipoko.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni