WAZIRI wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, ameendelea kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi na
mipaka baina ya wananchi na hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini
Waziri wa Maliasili na utalii (katikati) akisikiliza maelezo kutokakwa Afisa wa wanyama pori. picha kwa hisani ya mtandao.
Tayari Nyalandu amefanikiwa kumaliza migogoro ya mipaka baina ya wananchi
wa Mbarali ambao walikuwa na mgogoro mzito ulidumu kwa zaidi ya miaka saba na
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wananchi wa Bagamoyo na Hifaddhi ya Taifa ya Saadani
na sasa amegeukia mgogoro wa Misitu wa Marah na wananchi wa Kata ya Buger
wilayani Karatu.
Katika kuhakikisha
mgogoro unamalizika, Nyalandu alifanya ziara wilayani Karatu na kuunda Kamati
Maalumu itakayokuwa chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo Omar Kwaang’.
Wajumbe wengine wa kamati
hiyo watakuwa ni Ofisa Usalama wilaya, maofisa wa Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA) na wawakilishi wa wananchi.
Akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Bugher juzi, Nyalandu alisema
kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza uhusiano mbaya baina ya wananchi na
wahifadhi na kushauri njia sahihi itakayomaliza tatizo hilo.
Amesema kamati hiyo
itafanya kazi zake kwa wiki mbili na ilianza kazi rasmi juzi hiyo hiyo mara
baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi.
Awali, wananchi wa kata
hiyo walilalamikia vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari wa hifadhi
hiyo ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kubwa pindi wanapoingiza mifugo kuchunga
ndani ya msitu huo.
Akitoa malalamiko hayo
mbele ya Nyalandu, Elian Mboyah, amesema askari wa msitu huo wamekuwa na kawaida
ya kuwapiga pindi wanapowakuta ndani ya hifadhi na kudai kuwa wakati mwingine
silaha za moto hutumika.
Amesema wana imani kubwa
kuwa ujio wa Nyalandu kijijini hapo utakuwa suluhisho la mateso wanayoyapata na
kuomba, wahanga wa mateso ya wahifadhi hao wakaangaliwa kwa jicho la huruma
akiwa na maana ya kupatiwa huduma za kijamii.
“Tumekuona waziri
Nyalandu tuna imani mgogoro huu utakuwa na sura mpya ya amani na mahusiano
mapya…tumechoshwa kunyanyaswa na askari hawa. Tunaomba wahanga wa mateso
wakiwemo watoto, wajane na wazee wakaangaliwa kwani ndugu zao waliojeruhiwa
ndio walikuwa tegemeo,” amesema Mboyah.
Kwa upande wake, Nyalandu
amesema amesikia kilio cha wananchi hao na ndio sababu amefika eneo hilo kwa
lengo la kutafuta mwafaka na kwamba, wahifadhi ni watanzania waliojitolea
kulinda rasilimali, hivyo wasionekane kuwa maadui.
Amesema kuna kila sababu
kwa wananchi na wahifadhi kuwa na mahusiano mazuri yenye kujenga na kuonya tena
ni marufuku wananchi kupigwa ama mifugo yao kuteswa na kuuawa na kwamba atakayekiuka
agizo hilo, atachukulia hatua kali za kisheria.
Pia, Nyalandu alizulu
kaburi na kuzungumza na familia ya mwanakijiji anayedaiwa kupoteza maisha kwa
kupigwa na askari wa wanyamapori na kukabidhi ubani wa Sh. 3 milioni.
Katika kuimarisha ujirani
mwema na mahusiano mazuri baina ya wananchi na wahifadhi, Nyalandu alitangaza
kuipatia Kata hiyo Sh. 100 milioni kama mchango wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania
(TANAPA) kusaidia ujenzi wa madarasa.
Pia, alitangaza kutoa
Sh.60 milion ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa soko kwa ajili ya
kuwawezesha akina mama wajasiriamali kuuza bidhaa na kujiongezea kipato.
Awali, Mbunge wa Viti
Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema), amesema ujio wa Nyalandu utasaidia kumaliza
mgogoro huo na kuwataka wananchi kuweka itikadi za vyama pembeni na kuungana
kuhakikisha tatizo hilo linamalizika.
Katika ziara hiyo,
Nyalandu alifuatana na maofisa wa wizara, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA,
Allan Kijazi, ambaye aliongozana na maofisa wake mbalimbali, Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania, Herman Killario pamoja na wajumbe wa kamati ya
ulinzi na usalama wa wilaya ya Karatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni