Source: Mwananchi
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu juzi alizindua Mradi wa
Kuendeleza na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania utakaogharimu zaidi ya
Sh200 bilioni na unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Nyalandu alisema unatekelezwa baada ya
Rais Jakaya Kikwete kufanikiwa kuzishawishi nchi za Ujerumani, China na
Marekani.
Alisema nchi hizo zilikubali kushirikiana na Benki ya Dunia ili
kufanikisha mradi huo unaotarajiwa kunufaisha wananchi na nchi.
Alisema ukanda wa kusini ndiyo unaongoza kwa kuwa na vivutio vingi vya
utalii, lakini haviendelezwi na badala yake nguvu kubwa imekuwa
ikitumika katika vivutio vilivyopo ukanda wa kaskazini.
“Mradi huu utatekelezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa barabara, ukarabati wa madaraja, uboreshaji wa fukwe na
utunzaji wa vyanzo vya maji katika mikoa ya kusini,” alisema.
Alisema ni muhimu kuboresha sekta ya utalii kwa ajili ya maendeleo ya
nchi, hasa kwa kuzingatia kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 18 ya Pato
la Taifa na asimilia 25 ya fedha za kigeni zinazotokana na utalii.
Awali, katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru
alisema mradi huo ni wa miaka mitatu na utatekelezwa kwa awamu mbili.
“Katika awamu ya kwanza iliyokuwa ya maandalizi, Benki ya Dunia ilitoa
Sh5 bilioni na awamu ya pili ni utekelezaji zitatumika Sh200 bilioni.
Mikoa inayounda ukanda wa kusini ni Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi,
Mtwara, Iringa na Mbeya.
Alisema katika kutekeleza mradi huo, Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika na Wizara ya Maji ndizo zitakazohusika kusimamia mradi huo na
kuhakikisha unakuwa na faida.
“Tungependa kuona mradi huu unakuwa na manufaa kwa wananchi wa ukanda wa
kusini na nchi kwa jumla, sasa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha
anashiriki katika kuuboresha,” alisema Meru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni