Jumatatu, 29 Juni 2015

Utalii waongoza kuliingizia Taifa fedha za kigeni



Arusha. 
Na Filbert Rweyemamu ,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema pamoja na changamoto zinazolikabili Taifa ya kupiga vita ujangili unaohatarisha uwepo wa tembo nchini,bado sekta ya utalii inaongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (kulia) akimkabidhi Cheti na Tuzo Mwanasheria wa kampuni ya Zara Tanzania Adventure, Mwasiti Juma iliyotolewa na Taasisi ya Traveler's Eye kwaajili ya kuhamasisha Utalii Endelevu nchini. Katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha. katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya TraveleEye,William Mushi. Picha na Filbert Rweyemamu

Alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akitoa tuzo kwa taasisi mbalimbali barani Afrika zilizotambuliwa kwa kufanya utalii endelevu, hali inayohakikisha utunzaji wa mazingira, utalii wa kiutamaduni na kupiga vita ujangili.
Nyalandu alisema kuna ongezeko la idadi ya tembo kwenye mfumo wa ikolojia ya Hifadhi za Taifa ya Serengeti, Manyara na Tarangire licha ya idadi yao kupungua Ruangwa na Ruaha. Alizitaja nchi za Marekani, Ujerumani na China kuwa ni mfano wa kuigwa kwakuwa zimeendelea kusaidia sekta ya utalii nchini kupiga hatua na kuweka mazingira mazuri ambayo matokeo yake yanaonekana.
Mkurugenzi wa taasisi ya Traveler’s Eye,Yvonne Baldwin alisema Tuzo wanazotoa zinalenga kuzifanya kampuni za utalii na taasisi za uhifadhi kuwa na mitazamo tofauti na kuanza kuwa na utalii unaolenga vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Allan Kijazi alisema shirika hilo hutenga Sh70 bilioni kila mwaka kwa ajili ya shughuli za uhifadhi nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni