Daniel Mjema
Moshi.
Mwafrika wa kwanza kupanda Mlima Everest, Sibusiso Vilan ametaka
upandaji wa Mlima Kilimanjaro utumike kuwaunganisha Waafrika na mataifa
mengine duniani.
Vilan ambaye ni raia wa Afrika Kusini, alipanda mlima Everest ambao ni
mrefu duniani mwaka 2003 na kuwa Mwafrika wa kwanza kufika kileleni
mwaka 2005.
Mpanda mlima huyo wa kimataifa alitoa kauli hiyo juzi wakati yeye na
wenzake walipoanza safari ya siku sita ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa
ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia afya ya watoto wa kike.
Kwa sehemu kubwa fedha hizo zitasaidia watoto wa kike 272,000 wa Afrika
Kusini pia wa Tanzania wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya
Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Mbali na kupanda mlima huo kupitia taasisi ya Rais wa zamani wa Afrika
Kusini, Nelson Mandela ya Trek4 Mandela kuchangisha fedha, pia wanapanda
mlima huo kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwake kiongozi huyo aliyefariki
dunia mwaka juzi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada wa taulo kwa wanafunzi wa kike wa
Shule ya Msingi Mazoezi, Vilan alisema mlima huo ni hazina ya dunia
ambayo inaweza kuwaunganisha.
Katika hatua nyingine, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa),
limewaalika waandaaji wa tamthilia mashuhuri ya Isidingo, kuja kuandaa
tamthilia hiyo katika hifadhi za taifa nchini.
Mwaliko huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Utalii na Masoko wa Tanapa,
Ibrahim Mussa wakati wa tukio la kupanda mlima kwa wapandaji 37 kutoka
Afrika Kusini.
Miongoni mwa wapandaji hao ni waigizaji maarufu, akiwamo mwigizaji wa
tamthilia inayopendwa Afrika ikiwamo Tanzania ya Isidingo, Rajesh Kumar.
Mussa alimwomba Kumar kuangalia uwezekano wa kurekodi tamthilia hiyo
katika moja ya hifadhi za taifa nchini kwani hiyo pia itasaidia
kuutangaza mlima Kilimanjaro kimataifa.
Kumar alipoulizwa kuhusu mwaliko huo , alisema ataufikisha kwa waandaaji
ambao ni Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC). Mkurugenzi Mkuu
wa Tanapa, Allan Kijazi alisema tukio la upandaji linalofanywa na Trek4
Mandela litasaidia kuwaunganisha waafrika kwa vile wapandaji sasa
wanatoka mataifa mbalimbali.
Mwanzilishi na Mwasisi wa Trek4 Mandela, Richard Mabaso alisema lengo ni
kuchangisha fedha zitazowezesha kuwafikia watoto wa kike 272,000 wa
Afrika Kusini na Tanzania.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni