
Chakula kama hiki ni Maarufu kwenye Hoteli nyingi nchini.
Charles Kayoka
Dar es Salaam.
Moja ya mambo yanayotajwa kuwa yanaweza kuongeza pato kutokana na sekta
ya utalii ni watalii wa ndani ya nchi kuongezeka. Yaani hata wananchi
wenyewe kuwa watalii wa vivutio.
Hata hivyo, mimi ninaona kuna kasoro kidogo katika ainisho hilo la
watalii wa ndani. Tunawataja watalii wa ndani kama makundi ya watu
waliojiunga au kufanya uamuzi, kwa ajili ya kutembelea vivutio vya
utalii hasa, hifadhi za taifa na maeneo yaliyoainishwa kuwa ni ya utalii.
Hili ainisho ni moja. Hebu tumwangalie huyu msafiri anayekwenda sehemu
fulani kwa ajili ya kumtembelea ndugu yake au kwa ajili ya kufanya
mkutano. Huyu sio mtalii kwa maana ya ainisho la kwanza.
Tunaweza kujiuliza: Je, eneo analokwenda lina vivutio gani ambavyo
msafiri huyu anaweza kwenda kuvitembelea wakati akiwa likizo au
matembezi hayo?
Kwa sababu utalii sio lazima uende hifadhi za wanyama za taifa au maeneo
ya kihistoria. Nilidhani kuwa mtalii wa hivi anaweza kutembelea maeneo
yalifanyiwa kazi na kuanishiwa kuwa ni ya kitalii.
Kwa mfano kama Serikali imewekeza makumbusho ya wilaya husika, kuna
uwezekano wa watalii, wasafiri na wakazi wa eneo wakavutiwa kufika.
Wageni mara nyingi huwa na udadisi wa kutaka kujifunza na kutaka kuona
mengi katika eneo fulani.
Kwa hiyo kwa malipo wanaweza kutembelea makumbusho ya Halmashauri.
Lakini kila wilaya ina kivutio chake, wanyama, matunda, na vyakula
mbalimbali.
Kwa ubunifu halmashauri inaweza kuanzisha, kwa mfano, utalii wa chakula
kwa kutenga maeneo maalumu na vyakula vya eneo husika vikapikwa kwa
mapishi ya kienyeji katika hali ya usafi na kisasa.
Wasafiri hao au wenyeji wa eneo wanaweza kutembelea eneo hilo kula na
kujifunza mengine. Maeneo kama ya Dodoma Mnadani ni mfano mzuri, lakini
haujatumiwa vizuri sana kama kivutio cha utalii wa ndani wa chakula.
Ifike mahali wageni wa ndani na wa nje waseme, ukienda mahali fulani ni
vizuri ukafika eneo fulani kwa sababu kuna kivutio fulani, au kuna
matukio fulani ya kitalii.
Kwa hiyo utalii wa ndani si lazima uwe wa kutembelea wanyama au maeneo
ya kihistoria na kuwa faida ya kipato inaweza kuwa kwa wananchi wa
kawaida au Halmashauri za wilaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni