Arusha.
Mussa Juma
Katika hali ya kawaida, Watanzania wamezoea kusikia au kuona
vituo vya kulea watoto yatima, ambavyo vimesambaa karibu nchi nzima.
Vituo hivyo vinalea watoto yatima ambao wazazi wao ama wamefariki dunia
na kukosa wasimamizi wa familia au kutelekezwa na wazazi.
Baada ya kukithiri kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi,
vilianzishwa pia vituo vya kuwalea watoto wenye albinism.
Hatua hizo, zilichukuliwa ili kulinda maisha ya watoto,hao ambao walikuwa wakivamiwa na kukatwa viungo hata kuuawa na watu wenye imani za kishirikina.
Hata hivyo, baada ya jitihada za Serikali na wadau wengine, mauaji hayo
yamedhibitiwa, hivyo watoto kuanza kurejeshwa kwenye makazi yao.
Kurejeshwa kwenye makazi kwa watoto hao, kunatokana na sababu za
kitaalamu kuwa kuwalea wakiwa peke yao ni aina nyingine ya kuwatenga,
hivyo kuwafanya kuiogopa zaidi jamii inayowazunguka.
Yatima wa tembo
Hata hivyo, katika hali ianyoweza kustaajabisha, Tanzania sasa imeingia
katika historia nyingine kwenye sekta ya utalii kwa kuamua kuanzisha
vituo vya kulea watoto yatima wa tembo. Tayari kituo hicho cha kipekee
kimeanzishwa ili kulea watoto yatima wa tembo, jijini Arusha, jirani na
uwanja mdogo wa ndege.
Kituo hicho kimeanzishwa na Taasisi ya African Wildlife Trust kwa lengo
la kunusuru maisha ya watoto wa tembo ambao wazazi wao wanauawa na
majangili.
Kituo hicho kina vitanda maalumu vya kulala tembo, eneo la kupumzika na
eneo dogo la kutembea.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Pratik Patel anasema amekianzisha kwa
kushirikiana na wadau wengine ili kuokoa maisha ya tembo nchini.
Anasema tembo watoto, ambao wamekuwa wakipoteza wazazi wao kutokana na
kuuawa na majangili, wamekuwa pia wakifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ndiye aliyezindua kituo
hicho ambapo alieleza kuwa ni faraja kwa Watanzania kuwa na kituo cha
aina hiyo.
Anasema nchi nyingine zenye kituo kama hicho ni Kenya na Afrika Kusini.
Nyalandu anasema Serikali inaunga mkono jitihada zozote za kuokoa maisha
ya tembo, hata kama ni mmoja.
Anasema kituo hicho, kitaendeshwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya
Wanyamapori Tanzania.
“Kituo hiki kimeanzishwa wakati, natoa matokeo ya sensa ya tembo mwaka
2014, ambayo inaeleza kuwa waliopo nchini kwa sasa ni 43,330,” anasema
Anasema idadi hiyo imeongezeka kidogo, kutokana na ukweli kuwa tembo
walikuwa wamepungua katika maeneo ya ndani na nje ya hifadhi.
Waziri Nyalandu anasema, tembo watakaolelewa watatunzwa na wakikuwa
watarejeshwa kwenye makazi yao ya asili.
“Tunataka kuokoa japo tembo mmoja, lengo la Serikali kwa kushirikiana na
wadau wetu, miaka 15 ijayo waongezeke na kufikia 100,000,” anasema
Nyalandu.
Tembo wamepungua
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Dk Simon Mduma
anasema katika utafiti waliofanya kati ya Mei na Novemba mwaka jana,
imebainika tembo kupungua kwenye baadhi ya maeneo na sehemu nyingine
kuongezeka.
Anasema historia inaonyesha kwamba Tanzania iliwahi kuwa na tembo zaidi
ya 300,000, lakini sensa ya mwaka 2006, walibaki 132,000, mwaka 2009
walibaki 109,000 na sasa wamebainika wapo 43,330.
Wadau wapinga kituo
Wahifadhi wa Wanyamapori, Chama cha Waongoza Watalii (TTGA) na Kituo cha
Utafiti wa Tembo Duniani kilicho nchini (WEC) wanaonyesha shaka kuhusu
kituo hicho.
Makamu Mwenyekiti wa TTGA, Khalifa Msangi anasema wanahofu kubwa na
kituo hicho kwani kinaweza kuwa ni mpango wa kuanzisha eneo la kutunza
wanyama mjini (Zuu).
“Kama lengo ni kuwasaidia watoto wa tembo, kwa nini kituo hicho
kisingajengwa porini, kwenye maeneo ya asili ya tembo?” anasema.
Anaongeza: “Sisi ni wadau wakubwa wa utalii , tumelijadili suala hili
kwenye vikao vyetu na tumekuwa na wasiwasi mkubwa kwa nini kijengwe
mjini na katikati ya Arusha?
Je, tembo wakiwa wakubwa watawezaje kurejea porini na kuishi maisha yao
ya kawaida kwani muda wote wamekulia mjini?”
“Sisi ni wahifadhi tulitarajia wanyamapori wasaidiwe porini kwani huko
ndipo wamezaliwa, kuwaleta mjini ni kuwatenga... kama vituo vya yatima
vinafungwa ili watoto walelewe kwenye jamii zao iweje tembo tuwaanzishie
vituo vya kuwalea mijini,” anasema
Mkurugenzi wa WEC, Dk Alfred Kikoti anasema ni hatari kuanzisha vituo
vya kulea tembo bila kufanyika utafiti wa kutosha.
Hata hivyo, anasema kwa kuwa Serikali ndiyo iliyozindua kituo hicho,
anaamini kimesajiliwa na wamiliki wamefuata sheria .
“Hili si jambo geni duniani, lakini nilidhani juhudi zingefanywa katika
kulinda tembo, hasa ukanda wa kusini mwa nchi kwenye ujangili mkubwa,”
anasema
Anasema hata kungekuwapo sababu ya kujenga kituo hicho, kilipaswa
kujengwa ukanda wa kusini, hasa Mikumi ambako kuna tembo watoto wengi
ambao wazazi wao wameuawa .
“Suala hili lingeshirikisha wadau wengi hasa wahifadhi na watafiti
lingekuwa na dhamira njema zaidi,” anasema.
Mhifadhi John Macha anasema watalii wanapaswa kwenda kwenye hifadhi za
taifa na kuruhusu vituo vya aina hii, wanyama kama tembo wanaweza
kuwekwa huko ili waje kuona na kurejea makwao.
“Naweza kusema hii ni kama aina nyingine ya ujangili tu, kwani suala
hili linahitaji ushirikishwaji mkubwa wa wadau,” anasema
Macha anasema kwa mujibu wa sheria ya hifadhi za taifa, hairuhusiwi
kuchukua kitu chochote ndani ya hifadhi na kukipeleka nje ili kulinda
ikolojia ya hifadhi.
“Ndiyo sababu hata kinyesi cha tembo hakitakiwi kuchulikuwa. Ukikuta
mnyama kagongwa na gari, huwezi kumchukua kwani maisha ya hifadhini
mambo hutegemeana,” alisema.
Hata hivyo, swali linalobaki ni: Je, kituo hicho kitasaidia mapambano
dhidi ya ujangili au kuibua migogoro mingine katika sekta ya utalii?
Big Brother winner, Idris Sultan acquires new house...
Read More at thenet.ng/2015/01/photos-big-brother-winner-idris-sultan-acquires-new-house/ Follow us: @theNETng on Twitter | theNETng on Facebook
Read More at thenet.ng/2015/01/photos-big-brother-winner-idris-sultan-acquires-new-house/ Follow us: @theNETng on Twitter | theNETng on Facebook
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni