Anthony Mayunga
Imekuwapo dhana kuwa unapozungumzia mtalii unamaanisha ni mtu kutoka nje
ya nchi, hasa Ulaya, anayekuja nchini kuona maliasili ya taifa kama vile
kutembelea mbuga za wanyama, mambo ya kale na kupanda mlima.
Hali hii inatokana na utamaduni wa jamii nyingi za Kiafrika kutojenga
utamaduni wa kutenga muda kwa ajili ya kutembelea vivutio vya kitalii.
Wanauchumi mbalimbali wanaamini kuwa sekta ya utalii nchini inaweza
kukua na kuongeza pato lake maradufu iwapo jamii itaelimishwa juu ya
utalii wa ndani.
Sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa na
inaaminika kwamba ingeweza kufikia asilimia 30 ya pato hilo kama
kungekuwa na mkakati wa pamoja wa kutangaza fursa zilizopo na kuhimiza
utalii wa ndani.
Utalii wa ndani uboreshwe
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CBA Tanzania, Julius Mcharo anasema Tanzania
ni nchi ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na hata
watalii mbalimbali duniani wamekuwa wakivutiwa na jinsi vivutio hivi
ambavyo vinapatikana katika mikoa mbalimbali ya nchi.
Mcharo anasema yeye binafsi amepanda Mlima Kilimanjaro na kuona jinsi
watalii wanavyofaidi vivutio hivyo ambavyo ni mali ya Tanzania lakini
wenyeji hawafaidiki.
Ili kukuza utalii wa ndani na kuwafanya wenyeji wafaidike, anasema ni
lazima kuwe na mikakati mizuri inayolenga pia kuongeza pato la taifa.
“Baadhi ya nchi barani Afrika, hivi sasa, zimeanza kuweka mikakati ya
kukuza na kuweka vipaumbele katika utalii wa ndani badala ya kukazia tu
utalii wa nje,” anasema Mcharo.
Anahimiza Watanzania kubadilika na kushiriki kwenye utalii badala ya
kubakia nyuma wakati wageni wanafaidika.
Vilevile, anasema Watanzania wakibadilika ni mapinduzi ya sekta ya
utalii kwa sababu itaachana na kutegemea wageni wa nje ambao wakati
mwingine hupungua na kusababisha mtikisiko wa mapato kisekta.
Kwa sababu hiyo anaihamasisha Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha
inaweka msisitizo katika kutangaza na kuhamasisha utalii wa ndani ili
kupunguza utegemezi kwa watalii wa kigeni.
Kwa kutambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika pato la taifa,
Mcharo anasema CBA Tanzania tayari imeanza kukopesha wafanyabiashara
wanaofanya biashara za utalii.
“CBA Tanzania itaendelea kubuni huduma mbalimbali za kukuza sekta ya
utalii nchini kwa upande wa utalii wa na ule wa ndani,” anasema.
Anawataka Watanzania kuchangamkia fursa kwa kuibua miradi mbalimbali ya
utalii na benki ya CBA Tanzania itafungua milango yake kwa kuwahudumia
Watanzania wenye lengo la kukuza sekta hiyo.
Anasema lengo la CBA Tanzania ni kuona upungufu katika mambo ya kitalii
nchini unaondoka na mambo yanaimarika ili kuvuta wageni wengi.
Anatoa mfano alipopanda Mlima Kilimanjaro alibaini kuwa bado kuna huduma
hafifu hasa vituo vya kufikia watalii kama vile hoteli na isitoshe
hakuna mipango mizuri ya huduma ya kwanza kwenye vituo na gharama za
kupanda mlima bado ni kubwa kiasi kwamba Mtanzania wa kawaida hatazimudu.
“Kuna jambo pia la hatari hasa panapokosekana chupa za hewa ya oksijeni
hasa mtalii anapokaribia kilele cha mlima ambako mzunguko wa hewa siyo
mkubwa na hivyo huathiri watalii katika kupumua,” anabainisha Mcharo.
Kudorora utalii wa ndani
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devota Mdachi anasema
kuwa kuna changamoto nyingi zinachangia utalii wa ndani kudorora.
Anataja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni bajeti ndogo ya utangazaji
inayotolewa kwa Bodi ya Utalii Tanzania. “Sekta hiyo ingefanya vizuri
iwapo Serikali ingekuwa inatenga fedha nyingi kwa ajili ya matangazo
kama ilivyo kwa nchi zingine zinazotuzunguka,” anasema Mdachi.
Anatoa mfano: “Kwa mwaka huu wa fedha, Tanzania imetenga Dola 2.7
milioni za Marekani sawa na Sh6.2 bilioni kwa ajili ya kutangaza utalii,
Kenya wametenga Dola za Marekani 36 milioni sawa na Sh82.9 bilioni za
Tanzania, Uganda Dola 3.9 milioni sawa na Sh9 bilioni za Tanzania.”
Anasema Tanzania yenye vivutio vingi duniani ndiyo nchi inayotenga
bajeti ndogo kwa ajili ya kutangaza fursa ilizonazo, matokeo yake bodi
haitekelezi mikakati yake ili kufikia lengo ili kukuza utalii wa ndani.
Pamoja na sekta hiyo kuchangia pato kubwa la Taifa, anasema haipo kwenye
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na siyo kipaumbele cha taifa.
Anasema changamoto nyingine ni pamoja na utamaduni uliojengeka kwa muda
mrefu kwa Watanzania kutotembelea vivutio vilivyopo, wakiamini kuwa
utalii unawahusu wageni kutoka nje na gharama kubwa za malazi katika
hoteli, hasa zilizoko kwenye hifadhi.
Kampeni utalii wa ndani
Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi anasema
shirika hilo limezindua kampeni ya miezi sita ya kuhamasisha utalii wa
ndani kwa kuwa unachangia ongezeko la pato la taifa. “Kwa upande wa
wageni wa nje wanakuja wengi na utalii endelevu ni ule ambao wazawa
wanashiriki kikamilifu,” anasema akibainisha kuwa si vizuri kutegemea tu
watalii wa nje.
Mcharo anasema Watanzania wanapaswa kufahamu pia kupanda mlima
kilimanjaro ni sehemu ya ukakamavu wa mwili licha ya kunufaika na mambo
utakayoshuhudia.
“Upandaji mlima ni mazoezi ya kujenga afya ya mwili na ni kivutio
kinachoburudisha na kufanya akili na mwili vitulie baada ya uchovu wa
kazi za muda mrefu,” anabainisha Mcharo.
Anasema yeye binafsi amekuwa akihamasisha utalii wa ndani ambapo yeye na
wenzake waliunda kundi Victoria Group na kutenga muda wao ili kupanda
mlima huo mrefu kuliko yote Afrika. Anasema upandaji wa Mlima
Kilimanjaro ulikuwa na changamoto nyingi zikiwamo za hali mbaya ya hewa.
Hata hivyo, anahimiza Watanzania kutembelea vivutio hivi ili waweze
kufurahia nchi yao ambayo ina raslimali nyingi za kustajabisha na
zinazowavutia wageni.
Nini kifanyike ili kukuza utalii wa ndani? Jibu ni kwamba Serikali haina
budi kutenga bajeti za kukuza utalii, nguvu ielekezwe katika kukuza
utalii wa ndani, somo la utalii liongezwe katika mitalaa ya shule za
msingi na tozo za kuingia kwenye hifadhi zipungue.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni