Daniel Mjema
Moshi.
Mwigizaji maarufu wa tamthilia ya Isidingo The Need, Jack
Devnarain maarufu kwa jina la uigizaji la Rajesh Kumar, amefanikiwa
kufika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro.
Rajesh, ambaye ni raia wa Afrika Kusini, pamoja na wenzake 36 walipanda
mlima huo kuanzia Julai 14, kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Hayati
Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Mbali na kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa Taifa la Afrika Kusini, pia
walipanda kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia afya za watoto wa
kike 272,000 wa nchi hiyo na Tanzania.
Mratibu wa Taasisi ya Mandela ya Trek4 Mandela nchini, Honest Minja
alisema jana kwamba Kumar na wapanda mlima wenzake 31 kati ya 37
walifanikiwa kufika kileleni.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus
Lufungulo alisema kati ya watu 37 waliopanda mlima, 32 walifika kileleni
na watano waliishia njiani.
“Wageni 32 wa Trek4 Mandela wamefika kileleni akiwamo msanii wa
Isidingo. Watatu waliishia kituo cha Kibo na wawili waliishia kati ya
Kibo na kilelele cha Gilmans,” alisema.
Kundi hilo la wapanda mlima lilimjumuisha mpanda milima wa kimataifa
Sibusiso Vilane ambaye ni Mwafrika wa kwanza kupanda mlima Everest ambao
ni mrefu kuliko yote duniani.
Jana walitarajiwa kushuka hadi Kituo cha Horombo kilichopo urefu wa mita
3,720 na leo walitarajiwa kushuka hadi Mandara mita 2,700 na baadaye
hadi lango kuu la Kinapa lililopo Marangu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni