Dar es Salaam.
Na mwandishi wetu.
Wizara ya Maliasili na Utalii imeahidi kuupa
kipaumbele mchakato wa kuifanya Bodi ya utalii Tanzania (TTB) kuwa Mamlaka ya
Utalii Tanzania (TTA) kwa lengo la kuiwezesha bodi hiyo kufanya kazi kwa
ufanisi na kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.Aidha Mamlaka hiyo imeitaka
TTB kuangalia ni maeneo gani yanayoweza kuwa vyanzo vya mapato
vitakavyoiwezesha bodi kupata fedha.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Maliasili na
Utalii,Dkt.Adelhem Meru alipotembelea makao makuu ya Bodi ya Utalii yaliyoko katika jengo la ISP jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na
wafanyakazi wa bodi hiyo.
Dkt.Meru ameipongeza bodi ya utalii kwa kuendelea
kufanya kazi vizuri katika mazingira
yenye changamoto nyingi hasa za kifedha.Amesema
TTB ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza vivutio vya utalii kwa ujumla wake , hivyo
kinapaswa kuwezeshwa kutimiza jukumu hilo kwa niaba ya nchi badala ya kila taasisi kutangaza vivutio inavyosimamia.
“Tunawajibika
kwa kuwawezesha TTB mtekeleze majukumu yenu vizuri kwa kuwa ninyi ndio
mliokabidhiwa jukumu la kutangaza vivutio vya utalii kama vile vya,fukwe,wanyama,historia ,milima nk” alisema.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Dkt.Meru kutembelea Makao
Makuu ya Ofisi ya Bodi ya Utalii tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo,Bodi ya
Utalii ni moja ya taasisi zilizoko chini
ya wizara yake yenye jukumu la kutanga vivutio vya utalii vya Tanzania ndani na
nje ya nchi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni