Antony Mayunga
Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (Tawiri) na
Tanzania Elephant Protection Society (TEPS), mwaka 2012 walitoa taarifa
iliyoonyesha kuwa wastani wa tembo 30 hufa kwa siku, kwa mwezi ni 800 na kwa
mwaka inakadiriwa kufikia 10,000.
Licha ya kukinzana, mipango mbalimbali imekuwa
ikifanywa ili kudhibiti tatizo hilo ambalo linatishia kumaliza tembo, wanyama
ambao ni adimu na walio kivutio kikubwa cha utalii.
Takwimu hizo za kitafiti zinafuatiwa na
zilizofanyika Oktoba hadi Desemba 2013 katika eneo la Selous, pamoja na kuwapo
kwa taarifa za ongezeko la tembo katika maeneo ya Serengeti.
Kwenye hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Desemba
31,2014 katika salaamu za kufunga mwaka na kukaribisha mwaka mpya 2015
alizungumzia pia juu ya ujangili.
Rais anasema mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikiwa
ni sawa na ndovu 9 kwa mwezi kwa nchi nzima ukilinganisha na 219 waliouawa mwaka
2013 na mwaka 2012 ndovu waliouawa walikuwa 473.
Majangili 1,354 walikamatwa, pembe za ndovu 543 na
silaha 184 zilikamatwa kwa kipindi hicho na kuwa ujangili kwa sasa umepungua,
ingawa majangili waliofungwa kama kiashiria cha hatua kuchukuliwa hakusema.
Takwimu hizo zinaonyesha kushuka kwa asilimia
kubwa kwa kuwa mwaka 2012 taarifa za utafiti wa taasisi za ndani na nje
zilibaini kuwa tembo 10,000 kwa mwaka.
Januari 2014, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Waziri, alitoa takwimu za
sensa ya wanyama iliyofanyika Oktoba hadi Desemba 2013 katika eneo la Selous
kuwa mizoga 6,516 ilihesabiwa ambayo ni zaidi ya mara ishirini na tisa ya
takwimu zilizotolewa na Rais Kikwete.
Kwa kipindi hicho Mizoga ilibainika katika eneo la
ikolojia ya Selous, Mikumi, Ruaha na Rungwa, tafiti zilibaini asilimia saba
hadi nane ya mizoga hiyo ilitokana na vifo vya asili, kama ugonjwa na uzee,
lakini asilimia 92 ikiashiria vilisababishwa na ujangili.
Kwa mujibu wa utafiti ulioshirikisha wataalamu wa
ndani na nje kwa kufadhiliwa na Shirika la Misaada ya kiufundi la Ujermani
(GIZ), Frankfurt Zological Society (FZS) na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Tanapa na Spanest, ulibaini
ujangili wa kutisha.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa hali ilivyokutwa
katika pori tengefu la Kilombero ambalo ni sehemu ya ikolojia ya Selous na
Mikumi mwaka 2002 lilikuwa na tembo 2,080 wakati wa sensa ya mwaka 2013
hakukuwa na tembo hata mmoja, lakini taarifa zinazotoka sasa zinaonyesha
ujangili umepungua.
Kwa mjibu wa wizara ya Maliasili na Utalii
viashiria vingine vya ongezeko la ujangili ni kasi ya kukamatwa kwa meno ya
tembo kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi septemba 2013 meno yenye uzito wa
kilogramu 32,987 yalikamatwa ndani na nje ya nchi.
Uhasama
unachochea ujangili
Matokeo ya tafiti hizo zinazoonyesha ukubwa wa
tatizo ndiyo chanzo cha kuwekwa mikakati mingi iliyopata misaada ya mataifa
mengine ya nje ili kusaidia kukabiliana na ukubwa wa tatizo hilo linalotishia kumaliza
rasilimali hizo ni ushirikishwaji wa jamii.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa mjini Gabarone
Botswana Desemba mwaka 2013 na Mkutano wa London nchini Uingereza Februari
2014, uliazimiwa kwamba ipo haja ya kushirikisha wananchi waishio kandokando ya
maeneo ya hifadhi.
Hii inatokana na ukweli kwamba wanaoishi karibu na
hifadhi ndio mara nyingi wamekuwa wakijua baadhi ya wanaojihusisha na biashara
hiyo na hata mbinu ambazo wanatumia lakini wamekuwa wakificha taarifa hizo.
Ni ukweli usiopingika kwamba hata hapa nchini,
baadhi ya watu wanaoishi jirani na hifadhi wamekuwa hawana uhusiano mzuri na
mamlaka zinazosimamia mali hizo asili.
Moja ya tatizo ni unyanyasaji unaofanywa na baadhi
ya askari ambao wanalinda hifadhi. Wengi wao wamekuwa wakionekana jeuri na
huwapiga na hata kuwajeruhi baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kwa madai kwamba
wameingia maeneo ya hifadhi au wanyama wao, kama vile ng’ombe, walionekana
maeneo hayo.
Mtafiti wa Wanyamapori, Mabenga Magonera anasema
wakazi wengi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti wamekuwa hawana
uhusiano mzuri na hifadhi kutokana na kasoro kadhaa.
Miongoni mwa kasoro hizo anasema ni tozo za kodi
ambazo zinaonekana kuwaongezea gharama bila sababu pamoja na ugomvi wa mara kwa
mara hasa pale inapotokea mwanakijiji kaingia kuokota kuni kwenye hifadhi.
Magonera anaelezea tatizo la kodi wakazi wa
Serengeti kuwa hutokea pale wanapopita wakitoka au kuingia vijijini kwao
wanapokuwa na safari za wilaya au mikoa mingine.
Anasema hata kama ni mgonjwa anapelekwa hospitali,
kwa mfano mara nyingi huwapeleka hospitali za Arusha, hulazimika kulipia
Sh3,000 wanapokatiza Serengeti na Sh5,000 kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.
“Hii ni uonevu na inawanyanyasa wakazi wa
Serengeti na hata bidhaa zinazowafikia zinakua aghali kutokana na kodi hizi,”
anasema akisisitiza zilipaswa kulipwa na watalii na si wapita njia.
Anahoji ni kwa nini kodi za namna hiyo hazitozwi
kwenye Mbuga ya Mikumbi ambamo imepita barabara ya Dar es Salaam kwenda mikoa
ya Nyanda za Juu Kusini.
Mambo mengine ambayo yanaonekana ni manyanyaso kwa
wakazi wa vijiji vya Wilaya ya Serengeti ni kukamatwa na kushtakiwa wilaya ya
jirani ya Bunda inapotokea wamekutwa wakikata nyasi, kuni au miti ya
kutengeneza nyumba.
“Wanaenda kuwashtaki Bunda, umbali wa kilomita
150, wakati wilayani Serengeti kuna mahakama za ngazi hiyohiyo ya wilaya. Hii
ni kwanyanyasa! Wanafanya hivyo ili wananchi wapate usumbufu wa kwenda mbali
kusikiliza kesi, kupoteza muda na wanaathirika kiuchumi kwa sababu kazi zao
zinasimama. Hii ni kuwafanyia ukatili ili washindwe kuomba dhamana. hili
linapaswa kukomeshwa!” anaonya Magonera.
Tatizo jingine anasema ni la barabara kutokuwa na
lami kwa madai ni kutoathiri hali halisi ya hifadhi, jambo ambalo linafanya
usafiri kuwa mgumu, wenye gharama kubwa na hata kuongeza gharama za bidhaa.
Anasema Serengeti haijaunganishwa kwa barabara ya
lami kama ilivyo wilaya nyingine nchini. Pamoja na kwamba kumekuwepo na
shinikizo la kuzuia barabara kujengwa ndani ya eneo la hifadhi, lakini kuna
maeneo ya wilaya yanaweza yakatengenezwa ni kupunguza adha.
Mikakati mingine inatajwa kuwa ni utoaji wa elimu
ya namna ya kudhibiti vyanzo vya ujangili na kufanya kazi kwa ushirikiano na
wadau wengine wa maendeleo, taasisi za uhifadhi, mashirika yasiyokuwa ya
kiserikali, serikali, watafiti na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Ili vita ya kupambana na ujangili iwe na nguvu,
takwimu zinatakiwa kuwa sahihi na kuwapo, mkakati makini kukabili ujangili na
kuepuka chokochoko na wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni